Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewataka wataalamuu wa Mabwawa na watumishi wengine wa wizara hiyo, Jijini Arusha Kutafuta Jitihada za haraka za Kunusuru bwawa la Nanja lililomeguka Jijini Arusha.
Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha kumeguka kwa sehemu ya ukuta wa Bwawa hilo ambalo ni tegemeo kama chanzo cha maji kwa vijiji zaidi ya thelathini Mkoani humo.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa kata za lepruko, sepeko na Mkuyuni Jijini humo na kusisitiza umuhimu wa bwawa la Nanja kwa vijiji vinavyozunguka bwawa hilo.
Waziri Aweso amesisitiza kwamba pamoja na ugumu wa kukarabati bwawa hilo likiwa na maji, anawataka wataalamu wa wizara ya maji kufanya maamuzi magumu na kutumia uwezo wao wa kitaaluma kufanikisha zoezi hilo.
Amewataka watalaamu hao kuhakikisha wanafanya ukarabati wa haraka ili kudhibiti maji yasiendelee kupotea pamoja na kufanya usanifu wa kina ili ukarabati wa uhakika uweze kufanywa kipindi cha kiangazi.
Kwa upande wa Mbunge wa Monduli Fredrick Lowassa amesema, bwawa hilo la Nanja ndio tegemeo la wakazi wa Monduli kwenye matumizi ya maji kwa binadamu, mifugo na wanayamapori.