Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameamua kukutana na kuongea na Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo leo ambapo tayari amefika Kariakoo muda huu badala ya Jumatano May 17,2023 ambayo ilitangazwa hapo wali hii ni kutokana na uzito wa suala hilo.
Awali mkutano kati ya Waziri Mkuu na Kamati ya Wafanyabiashara hao pamoja na TRA na Mawaziri wa Sekta husika ulitarajiwa kufanyika saa 8 Mchana kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu Magogoni-Ikulu Dar es salaam Jumatano May 17, 2023 kwa uratibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala, lakini Waziri Mkuu ameamua aende leoleo Kariakoo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuna taarifa za uwepo wa kikosi kazi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania ambao wanakusanya kodi kwa wafanyabiashara huo, ameagiza kiondolewa kwani ni kinyume na maaagizo ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tunazo taarifa kuwa kuna kikosi kazi kimeundwa kinazunguka humu ndani (Kariakoo) pamoja na kazi nzuri inayofanywa katika kukusanya kodi lakini Rais Samia Suluhu Hassan alikemea suala la kikosi kazi (task force),” amesema.
Aidha, Majaliwa amemuagiza Kamishna wa makusanyo ya ndani kusitisha kikosi kazi hicho na kama kuna ulazima basi ni lazima Waziri wa Fedha afahamu.