Thamani ya Dola ya Kimarekani dhidi ya Shilingi ya Tanzania imefikiwa kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu kuanza kutumika kwa sarafu hizo.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya soko la fedha hapa nchini, jana dola moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh2,550 na ikinunuliwa kwa Sh2,510, jambo ambalo limeibua wasiwasi miongoni mwa watu, hususan wanaotumia sarafu hiyo katika manunuzi.
Tangu Oktoba mwaka jana dola ya Kimarekani ambayo hutumiwa katika miamala ya kimataifa kwa asilimia 85 imekuwa ikiimarika dhidi ya sarafu nyingine, jambo ambalo linatajwa kusababishwa na sheria ya kupambana na mfumuko wa bei iliyopitishwa na Taifa hilo la kwanza kiuchumi duniani.
Akizungumzia mwenendo unaokuwa wa thamani ya dola dhidi ya Shilingi, mchumi Dkt Jane Buberwa anayeishi Dar es Salaam alisema hali hii itasababisha ongezeko la bei kwa watumiaji wa chini.