Wakala Wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA wamekamilisha ujenzi wa daraja la chuma katika Mto Lwipa (Mabey Bridge) lenye urefu wa mita 27, pamoja na matengenezo ya barabara ya kutoka Kisegese kupitia Chiwachiwa hadihadi Lavena yenye urefu wa Km 15 kwa gharama za Sh bilioni 1.8.
Kukamilika kwa daraja hilo limewezesha kuunganisha Kata Mbingu na kata ya Namwawala katika Halmashauri ya Mlimba, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro.
Meneja wa TARURA, Wilaya ya Kilombero Mhandisi Sadiki Kalumi amesema faraja hilo lilijojengwa na wataalamu wa TARURA litarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji katika maeneo hayo.
“Daraja hili lina urefu wa mita 27 limegharimu shilingi milioni 900, lakini pamoja na daraja kuna matengenezo ya barabara ambayo itajengwa kwa kiwango cha changarawe pamoja na makalavati kwa gharama ya Sh milioni 900 kufanya jumla ya gharama kufika Sh bilioni 1.8” Ameongeza Mhandisi Kalumi.
Mhandisi Sadiki amesema hapo awali wananchi walikuwa wakitumia gogo kuvuka mto huo, Baadae lilijengwa daraja la mbao ambalo pia halikuwa la uhakika.
Na baada ya kuonekana kero hiyo katika usafirishaji ndipo ulipokuja mradi wa kujenga daraja la chuma kwa kutumia wataalamu wa TARURA, ambayo wanatarajia itachochea shughuli za kilimo katika maeneo hayo ya Chiwachiwa na Kisegese.