Tanzania imepokea makampuni zaidi ya 20 kutoka kwenye mataifa mbalimbali duniani ambayo yameingia mkataba wa kufanya uwekezaji katika biashara ya hewa ya Kaboni unaotarajiwa kuwa wa thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 10.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo jana alipokuwa akifunga mdahalo wa masuala ya biashara ya hewa ya Kaboni jijini Dar es Salaam.
“Mpaka sasa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake zimepokea makapuni zaidi ya 20 kutoka nchi za Kenya, Urusi, Singapore, Marekani, Kanada, Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Uswisi, Estonia, na Italia kuja kuwekeza katika biashara ya hewa ya Kaboni,” amesema Naibu Waziri Masanja.
Aidha amesema nchi hizo zimeshaingia makubaliano ya awali na Tanzania na baadhi ya mazungumzo yanaendelea kwenye taasisi husika chini ya usimamizi wa Kituo cha Uratibu wa Masuala ya Hewa ya Kaboni kilichopo Mkoani Morogoro (NCMC).