Kutokana na utabiri wa hali ya hewa uliyotolewa na mamlaka ya hali ya hewa nchini Tanzani, kuna uwezekano wa kuwa na mvua kubwa juu ya wastani na uwepo wa Elnino kuaniza mwishoni mwa mwezi Septemba 2023 hadi January 2024.
Mvua hiyo ya Elnino inatarajiwa hasa kuwepo katika Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kigoma, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Wizara ya Afya imetoa rai kwa wananchi wa maeneo husika kuzingatia mambo yafuatayo ili kuepuka au kupunguza madhara ya kiafya yanayoweza kuletwa na mvua hiyo kubwa.
Epuka kukaa au kugesha usafiri chini ya miti mikubwa, vilevile wakati wa mvua kubwa kuna uwezekano wa mawe makubwa kuporomoka kutoka milimani au miti kuanguka na kuziba barabara hivyo madereva wanaaswa kuwa makini kwa kuendesha vyombo vyao kwa mwendo unaokubalika kwa kuzingatia alama za barabarani.
Pia, Usijikinge dhidi ya mvua kwa kusimama chini ya mti, usishike wala kukanyaga waya wa umeme uliokatika, watu wanaoishi mabondeni au karibu na fukwe wanatahadharishwa kuhama au kutafuta hifadhi kwa muda.
Aidha, mvua hizo kubwa zinaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa yanayohusiana na maji kama vile malaria, Dengue na magonjwa ya kuhara ikiwemo kipindupindu hivyo inashauriwa kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuchemsha maji ya kunywa au kuyatibu na dawa ya Klorini.