Serikali nchini Congo Brazzaville imezikosoa na kupinga tetesi za kuwapo kwa mapinduzi ya kijeshi nchini humo kama ilivyoripotiwa na mitandao ya kijamii.
Taarifa za nchi hiyo kupinduliwa na wanajeshi zilisambaa katika mitandao ya kijamii wakati Rais wa muda mrefu wa nchi hiyo, Denis Sassou Nguesso akiwa nje ya nchi kikazi.
Ufafanuzi huo umetolewa Jumapili usiku Septemba 17, 2023 na Waziri wa Habari, Thierry Moungalla aliyewatoa hofu wananchi na kuziita taarifa hizo kuwa ni uzushi.
“Tunaomba utulivu uendelee na watu waendelee na shughuli zao za kila siku,” ameandika Waziri huyo katika mtandao wake wa kijamii wa X.