Serikali imetangaza kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma na binafsi za Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku ifikapo Januari 31, 2024.
Sambamba na hilo, imezielekeza taasisi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 300 kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2025.
Akitangaza uamuzi huo wa serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Mhe Seleman Jafo alisema taasisi hizo zitatakiwa kutumia nishati mbadala ambayo ni safi kwa ajili ya kupikia.
Waziri Jafo amefafanua kuwa serikali imeweka nia ya kupunguza athari za kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi zitokanazo na matumizi ya kuni na mkaa kwa kupikia na tayari imeandaa Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.