Rais wa Urusi Vladimir Putin amemwambia Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kwamba hatahudhuria Mkutano wa G20 utakaofanyika Septemba 9 na 10, 2023.
India ni mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mwaka huu, ambao utafanyika katika mji mkuu wa Delhi ambapo viongozi mbalimbali wa G20 wanatakiwa kukutana.
Raisi Putin alimwambia Waziri Modi kwamba Waziri wake wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov atahudhuria mkutano huo kwa niaba yake.
Kundi la G20 ni umoja unajumuisha nchi 19 tajiri zaidi duniani pamoja na Umoja wa Ulaya na kwa sasa India inashikilia urais wa G20, ambao huzunguka kila mwaka kwa nchi wanachama.
Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unatarajiwa kuwa gumzo katika mkutano wa kilele mjini Delhi, ambapo viongozi wa dunia akiwemo Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak watakuwepo.