Mtumiaji wa mitandao ya kijamii kutoka Morocco amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kumkosoa mfalme kwenye mtandao wa ‘Facebook’ juu ya hatua ya Morocco kuboresha uhusiano na Israel.
Said Boukioud, mwenye umri wa miaka 48, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kuchapisha ujumbe kwenye ‘Facebook’ ambao unakosoa uhusiano wa Morocco na Israel kwa njia ambayo imetafsiriwa kama kumkosoa mfalme.
Morocco na Israel zilianzisha tena uhusiano wao mwezi Disemba mwaka wa 2020 kama sehemu ya makubaliano yanayoungwa mkono na Marekani.
Aidha wakili wa raia huyo El Hassan Essouni amesema kuwa hukumu iliyotolewa na mahakama ya Cassablanca ni kali na haieleweki.
Ameongeza kuwa licha ya mteja wake kupinga uhusiano wa Morocco na Israel lakini hakuwa na nia ya kumkashifu mfalme kwa kufanya hivyo.