Marekani imesema itawaruhusu washirika wake wa Magharibi kuipatia Ukraine ndege za kivita za hali ya juu, zikiwemo za F-16 zilizotengenezwa Marekani, katika kuimarisha zaidi Kyiv.
Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Jake Sullivan alisema Rais Joe Biden “aliwajulisha wenzake wa G7” juu ya uamuzi huo katika mkutano wa kilele wa umoja huo huko Japan siku ya jana.
Wanajeshi wa Marekani pia watawapa mafunzo marubani wa Ukraine kutumia ndege hizo hatua itakayosaidia kukabiliana na jeshi la anga la Urusi.
Raisi Volodymyr Zelensky alipongeza hatua hiyo kama ni uamuzi wa kihistoria kwani Ukraine kwa muda mrefu imekua ikitafuta ndege za teknolojia ya juu.
Aidha Marekani inapaswa kuidhinisha kisheria uuzaji upya wa vifaa vilivyonunuliwa na washirika na hatua hiyo itasafisha njia kwa mataifa mengine kutuma hifadhi zao zilizopo za F-16 kwa Ukraine.