Nchi ya Mali imeiondoa lugha ya Kifaransa kama lugha rasmi, hatua ambayo imechukuliwa zaidi ya miaka 60 baada ya Mali kupata uhuru wake.
Uamuzi huo umo katika katiba mpya ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi, iliyoidhinishwa Jumamosi.
Mahakama ya Katiba ya Bamako ambao ndio Mji Mkuu wa Mali ilithibitisha matokeo ya mwisho ya kura ya maoni ya mwezi Juni, ambapo ilitangaza kupata idhini ya asilimia 96.91 kutoka kwa wapigakura wakiunga mkono kuondolewa kwa lugha hiyo.
Kifaransa kitatumika kama lugha kuu ya kufanyia kazi, wakati lugha 13 za kitaifa zinazozungumzwa nchini humo zitakuwa zinatambuliwa rasmi kama lugha za kitaifa.
Lugha nyingine 70 za asili, kama vile Bambara, Bobo, Dogon, na Minianka, ambazo baadhi zilipewa hadhi ya lugha ya kitaifa kupitia amri ya Rais mnamo 1982, zitaendelea kutumiwa.
Mali imekuwa chini ya utawala wa jeshi tangu mapinduzi yaliyofanyika mwezi Agosti 2020 na Mei 2021 baada ya muongo mmoja wa kutokuwa na utulivu wa kisiasa uliokumbwa na uasi wa jihadi.