Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeendelea na zoezi la utambuzi wa eneo kwa ajili ya Ubunifu na Usanifu wa Miundo mbinu ya umwagiliaji katika Kituo Cha TARI-Hombolo.
Hii ni baada ya kamati inayohusika na Miundombinu ya umwagiliaji ya TARI kuhitimisha zoezi kama hilo siku ya Aprili 13, 2023 katika Kituo Cha TARI – Makutupora na kumkabidhi Mkandarasi Pro-Agra kwa ajili ya kuanza kazi.
Hatua hii ni utekelezaji wa bajeti ya Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuweka miundombinu ya umwagiliaji. Miundombinu hiyo imewekwa katika vituo vya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ili kuongeza uzalishaji wa Mbegu na shughuli za Utafiti.
Akizungumzia utekelezaji huu Meneja wa Kituo Cha TARI-Hombolo Dkt. Joel Meliyo ameishukuru Serikali na kusema kuwa kukamilika kwa mradi huu wa umwagiliaji utawezesha shughuli za Utafiti na uzalishaji. Shughuli hizo zilikuwa zikifanyika katika vituo hivyo katika msimu wa mvua pekee, na mradi huu utaweesha kufanyika kipindi chote cha mwaka bila kutegemea mvua.
Pia kwa upande mwingine Katibu wa Kamati ya umwagiliaji kutoka TARI-Makao Makuu, Bw. Erick Kaswaka amesema uwa Serikali imejenga miundombinu hiyo katika vituo 13 vya TARI.
Na Mhandisi mshauri wa mradi huo Mha. Elizabeth Mziray amesema eneo la Hombolo lina maji ya kutosha na vigezo vingine vinavyokidhi mahitaji ya kilimo cha umwagiliaji. Mbali na kuwa ni mhandishi mshauri katika mradi huo, pia Mhandisi Elizabeth Mziray ni mtafiti saidizi katika kituo cha TARI Uyole.
TARI-Hombolo ni Moja kati ya vituo 17 vya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),Na ni kituo mahususi kwa Utafiti, uzalishaji na usambazaji wa Teknolojia za Mtama, Uwele , ulezi na Alizeti.