Mabalozi kutoka mataifa 13 ya kigeni wenye balozi zao nchini Kenya wameonyesha wasiwasi wao kuhusu mauaji na ghasia nchini Kenya wakati wa Maandamano.
Kulingana na taarifa ya pamoja iliotumwa kwa vyombo vya habari , mabalozi hao kutoka Marekani na mataifa ya magharibi wameonyesha kushtushwa na matumizi ya risasi Pamoja na uharibifu wa mali wakati wa maandamano ya wiki iliyopita.
Katika taarifa yao wamewataka viongozi wa upinzani pamoja na wale waserikali kuwasilisha matakwa yao kupitia majadiliano ya kuleta amani ili kutafuta suluhu ya kudumu kwa lengo la kuhakikisha kuwa hakuna maafa zaidi.
Wameongezea kwamba wako tayari kusaidia juhudi za kupata suluhu ya haraka.
Hata hivyo wakati kauli hiyo inatoka leo, upinzani unatarajiwa kuongoza maandamano ya siku tatu dhidi ya serikali kuanzia kesho Jumatano hadi Ijumaa kuishinikiza serikali kufutilia mbali muswada wa fedha wa 2023.