Inasemekana watoto wengi nchini wana ufaulu hafifu wa masomo ya sayansi na hisabati, kutokana na kupungua uelewa darasani ambayo husababishwa na lishe duni.
Imeelezwa kuwa asilimia kubwa ya watoto wenye lishe duni, huyakwepa na kuyachukia masomo hayo wakiyaona magumu, kwa sababu yanahitaji uwezo mzuri wa kufikiri.
Taarifa hii ilibainishwa mwishoni mwa wiki na Ofisa Lishe wa Jiji la Mbeya, Itika Mlagalila kwenye kongamano la kuimarisha ufaulu na ustawi wa wanafunzi shuleni kupitia lishe bora.
Kongamano hilo la lishe toshelevu kwa wanafunzi lililoandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la HELVETAS.
Itika alisema kuwa, watoto waliokosa lishe bora huwa na uelewa mdogo darasani wanapofundishwa, na wakati mwingine huchukia kwenda shule na kuanza utoro hadi kuzorota zaidi kielimu.
“Masomo ya sayansi na hisabati si magumu ila yanahitaji uwezo wa kufikiri, na tafiti zinaonyesha watoto wenye lishe duni huyachukia masomo hayo” alisema.
“Ukosefu wa lishe toshelevu linaathiri mpaka ufaulu kwa watoto wetu kwa kuathiri uwezo wa kufikiri” aliongeza.
Wakati akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa aliwataka wadau wote kuhamasisha uchangiaji wa chakula shuleni kutekeleza sera ya elimu.
Naye Mganga Mkuu wa Jiji la Mbeya, Yesaya Mwasubila alisema kuwa wamebaini kuwa lishe duni mlo wa mchana kwenye shule nyingi.
Alisema katika shule nyingi watoto wanakula makande, na walipowahoji walimu walisema chakula hicho ndio kinapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu.
Jambo la kuwalisha watoto makande kwa kuwa ni gharama nafuu na rahisi kupatikana si sahihi, badala yake watoto wanatakiwa kuandaliwa chakula bora.
Na kuongeza kuwa watoto wanastahili kupata chakula chenye mchanganyiko wa makundi sita ya vyakula.
Makundi hayo ni wanga, mafuta, sukari, matunda, mboga na vyakula vya asili ya wanyama, na wanaendelea kutoa elimu kwa wadau ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki kuimarisha lishe ya watoto shuleni.
Ofisa wa HELVETAS, Judith Sarapion alisema mradi huo wa miaka mitatu tayari umeshafikia kata zote 36 za Jiji la Mbeya.
Jukumu kubwa likiwa kuelimisha umuhimu wa lishe bora kwa wanafunzi shuleni, kwa kuwahamasisha wazazi kuchangia chakula na upandaji wa bustani za mboga na matunda shuleni.