Kampuni ya Isra Gold Tanzania inayomilikiwa na wawekezaji kutoka Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imefungua kituo cha kusafisha dhahabu mkoani Geita chenye thamani ya Sh bilioni 4.2.
Uwekezaji huo ni matunda ya ziara ya Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan nchini UAE Februari 2022 ambapo alipata fursa ya kutembelea na kuinadi Tanzania kwenye maonesho ya Dubai Expo 2022.
Akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho kilichopo kata ya Lwamugasa wilayani Geita, Mkurugenzi wa Isra Gold Tanzania, Mostaq Ahmed amesema wamevutiwa na sera rafiki ya uwekezaji nchini Tanzania.
Amesema kituo (kiwanda) hicho kitafanya kazi ya kusindika udongo wenye madini ya dhahabu na kitakuwa na uwezo wa kusafisha tani 15 za dhadhabu kwa saa, ambapo kitafanya kazi kwa muda wa saa 24.
Aidha amebainisha kuwa uwekezaji huo ni mwanzo, na malengo ni kujenga vituo vingine vitano kabla ya mwaka huu kuisha na pia kuongeza vituo vingine 10 ndani ya mwaka 2024 ili kufikia jumla ya vituo 16.