Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kuimarisha demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari tangu alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaama, Kamala amegusia mambo makubwa yaliyofanyika chini ya Rais Samia ikiwa ni pamoja na kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani.
Mengine ni kuruhusu mikutano ya hadhara ya kisiasa ambayo ilikuwa imezuiwa kwa zaidi ya miaka mitano, kufungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa na kuimarika haki ya wananchi kujieleza na kupata habari.
Kamala anaendelea na ziara yake nchini Tanzania ambapo pia anatarajiwa kutembelea Makumbusho ya Taifa na kuweka shada la maua ikiwa ni kumbukumbu ya walioathiriwa na shambulio katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam mwaka 1998, pamoja na kutembea taasisi ya Tanzania Start-up Association.