Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Bo Li amepongeza serikali ya Tanzania kwa kudumisha utulivu wa kiuchumi katika nyakati ambao ulimwengu umepitia changamoto zilizosababishwa na athari za vita ya Ukraine pamoja na janga la UVIKO-19.
Li amesema, “Hatua za haraka zilizochukuliwa na Tanzania zilisaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kulinda uchumi dhidi ya athari za vita nchini Ukraine,” amesema alipohitimisha ziara yake nchini Tanzania.
Li amesema alivutiwa sana na nguvu na uhai wa uchumi wa Tanzania wakati wa mazungumzo yake na wawakilishi wa sekta binafsi, asasi za kiraia, na wadau wa maendeleo.
IMF imehimiza Tanzania kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani kupitia marekebisho ya kodi, ambayo yatasaidia kujenga nafasi ya bajeti inayohitajika kugharamia matumizi ya kijamii na kuongeza uwekezaji wa kipaumbele katika elimu, afya na sekta nyingine.
Wakati wa ziara yake nchini Tanzania, Li alifanya mazungumzo na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Gavana wa Benki Kuu Emmanuel Tutuba, na maafisa wengine wa ngazi za juu.