Mamlaka nchini Ethiopia imesema imekua ikifanya oparesheni dhidi ya hoteli, baa na maeneo mengine ya burudani katika mji mkuu wa Addis Ababa ambapo inadaiwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na ushoga vinafanyika.
Ofisi ya utawala wa amani na usalama ya Addis Ababa,imesema pia imekua ikichukua hatua dhidi ya taasisi ambazo vitendo vya ushoga vinatekelezwa.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa ‘Facebook’, mamlaka ya jiji hilo ilisema hatua hiyo ilikuja baada ya kuwa tayari imevamia nyumba za wageni na kutekeleza msako huo.
Aidha wananchi wametakiwa kutoa taarifa katika vituo vya polisi kuhusu vitendo hivyo, wakati serikali ikiendelea na msako katika maeneo mengine.
Mapenzi ya jinsia moja ni marufuku nchini Ethiopia, japo hakujawa na ripoti zozote za hivi karibuni za kesi au hatia zinazohusiana na vitendo vya ushoga.