Baada ya kuibuka kwa mjadala katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania, kutokana na serikali ya Marekani kwa ushirikiano na jumuiya za kimataifa kutoa msaada wa chakula kwa shule zilizopo mjini Dodoma. Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amesema kuwa waagizaji hawakupaswa kuleta msaada huo wa chakula kwani Tanzania ina chakula cha kutosha ikiwemo hazina ya kutosha ya mchele na maharage.
“Tumewaambia ile NGO, waambieni Wamarekani hivi, mchele upo maharagwe yapo nchi hii, zile fedha wanazotumia kuwapa wakulima wa Marekani wawape wakulima wa Tanzania. Tununue mchele kutoka Tanzania, maharagwe kutoka Tanzania, halafu hivyo virutubisho mnavyotaka kuweka tuwekee hapahapa wote tunaona”.
Bashe aliongeza pia kuna changamoto ya kutokua na ushirikishwaji katika miradi, na miradi mingi hujiendesha kivyake.
Ingawa haijatajwa NGO iliyoleta shehena hiyo ya vyakula vilivyorutubishwa, ila taasisi ya chakula na lishe Tanzania (TFNC) imeripotiwa kuingia mkataba na asasi ya kiraia ya Global Communities ili kusaidia katika kuhakikisha lishe kwa wanafunzi kwenye shule mbalimbali nchini.