Wizara ya Katiba na Sheria, imewakutanisha pamoja mawaziri wa sheria na wanasheria wakuu wastaafu na waliopo madarakani katika kikao chenye lengo la maoni yao kuhusu mchakato kupata Katiba mpya.
Waliohudhuria kikao hicho kilichofanyika leo Agosti 28, 2023 jijini Dar es Salaam, ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman akiwa kama Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Dkt Damas Ndumbaro amesema wameamua kukutana na viongozi hao ili kupata uzoefu wao kwa kuwa waliwahi kufanya kazi katika wizara hiyo, hivyo wana ufahamu na uelewa wa kutosha katika mchakato wa Katiba mpya.
Waziri huyo amebainisha kwamba wizara yake imeamua kuliweka kama kipaumbele namba moja suala la elimu ya Katiba kwa wananchi kwa sababu tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawaifahamu Katiba, wengine hawajawahi hata kuiona.