Hadi kufikia mwaka 2022 Tanzania ilikuwa na jumla ya maprofesa 226 kati yao 163 wakiwa ni maprofesa washiriki (Associate Professors) na 63 ni maprofesa kamili (Full Professors), Bunge limeambiwa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kusini, Dkt Oscar Ishengoma, aliyehoji ni maprofesa wangapi wanaozalishwa kila mwaka na ni wangapi wanastaafu kwa kipindi hicho.
Amesema Profesa ni ngazi ya kitaaluma ambapo Mhadhiri au Mtumishi wa Taasisi za Elimu ya Juu hufikia baada ya matokeo ya kazi za kitaaluma ikiwemo kufanya machapisho na ufundishaji.
“Hivyo kupanda cheo kwa mwanataaluma kunatokana na jitihada za mhusika katika ufundishaji, kufanya tafiti na kuchapisha maandiko yake katika majarida yanayokubalika kitaifa na kimataifa,” amesema.
Amesema kuongezeka kwa idadi yao kunategemea zaidi jitihadi za mtu binafsi katika utekelezaji wa majukumu yake na kukubalika kwa jitihada hizo kwa wanataaluma wenziwe kwa kuzingatia miongozo waliyojiwekea.