Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya hali mbaya ya hewa kwa siku tatu ambapo utabiri umeonyesha kuna uwezekano wa kutokea upepo mkali na mawimbi makubwa.
Taarifa iliyotolewa na TMA inaonyesha kuwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatano hadi Ijumaa kutakuwa na upepo mkali unaofikia kilomita 40 na zaidi kwa saa na mawimbi yanayofikia ukubwa wa mita 2.
Hali hii inatarajiwa kutokea katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi ikihusisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Dar es Salaam, Pwani na visiwa vya Unguja na Pemba.
Mikoa mingine ambayo inaweza kukumbwa na hali hii ya hewa ni maeneo ya ukanda wa ziwa Victoria ikihusisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu, Mara na maeneo ya ukanda wa ziwa Tanganyika katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.
Kufuatia hali hiyo TMA imetaka tahadhari kuchukuliwa hasa kwa wanaofanya shughuli zao baharini na ziwani wakiwemo wanaotumia njia hizo kusafiri.