Ugonjwa wa Kipindupindu umeibuka jijini Dar es salaam ambapo zaidi ya watu 10 wamethibitika kuugua ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Aprili 24, 2023 na Wizara ya Afya, ugonjwa huo ulibanika katika Kata ya Kivule Wilayani Ilala, ambapo wagonjwa saba walipimwa na kukutwa na vimelea vya ugonjwa huo, huku wengine watatu wakipatikana kutoka Kata za Tabata, Ilala na Buguruni.
Tangu kubainika kwa ugonjwa huo April 20, mwaka huu, mpaka sasa hakuna taarifa za kifo zilizotokana na ugonjwa huo.
Wizara inasisitiza kudumisha usafi katika maeneo ya biashara hasa yanayokutanisha watu wengi, kuosha mikono na kuchukua tahadhari zote muhimu kujikinga na kipindupindu.