Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa ameagiza kuondolewa kwa wataalam wote wanaosimamia ujenzi wa Barabara ya Kibaoni -Sitalike, sehemu ya kwanza ya Kibaoni-Mlele (km 50) kwa kiwango cha lami kutokana na ujenzi wa mradi huo kususua na utekelezaji wake kuwa nyuma kwa asilimia 23.71.
Ameagiza kuondolewa kwa wataalam wote wa Mhandisi mshauri wa mradi kutoka kampuni ya Crown Tech, Msimamizi wa Mradi kutoka Makao Makuu ya TANROADS, Mhandisi Ramadhan Myanzi pamoja na Msimamizi wa Mradi mkoa wa Katavi, Mhandisi Albert Laizer.
Bashungwa ametoa agizo hilo mkoani Katavi wakati akizungumza na wananchi wa kata ya kibaoni mara baada ya kukagua mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 14.7 na kutoridhishwa na kasi ya usimamizi na utekelezaji wa mradi huo.
“Mtendaji mkuu wa TANROADS ninakuagiza watumishi wote ambao wapo chini ya Crown Tech wanaosimamia mradi pamoja na msimamizi wa mradi kutoka TANROADS wote waondoke mara Moja, waje wapya, nataka hii kazi ifanyike usiku na mchana barabara hii ikamilike kama ilivyopangwa” Waziri Bashungwa.
Aidha Bashungwa amebaini ubovu wa mitambo ya Mkandarasi na Amemuagiza katibu mkuu wa Wizara ya ujenzi kupeleka timu ya wataalam kufanya ukaguzi wa mitambo na kutambua mingapi inafanya kazi na mingapi haifanyi kazi pamoja na kuchukua hatua za kimkataba kwa Mkandarasi na Mhandisi mshauri.