Kiongozi wa Palestina Mahmud Abbas amesema kwamba hakuwezi kuwa na amani katika Mashariki ya Kati bila suluhisho kati ya palestina na Israel.
Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo na kuitahadharisha Saudi Arabia ambayo Kwa sasa ina mpango wa kutambua utaifa wa Israeli.
“Wale wanaofikiri kuwa amani inaweza kutawala katika Mashariki ya Kati bila watu wa Palestina kufurahia haki zao kamili, na halali za kitaifa watakuwa wamekosea,” Abbas aliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kiongozi huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 87 alitoa wito wa mazungumzo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuitisha mkutano wa kimataifa kuhusu kuunda taifa la Palestina.
Marekani ina historia ya upatanishi wa amani kati ya pande hizo mbili, na Rais Joe Biden alizungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwenye Umoja wa Mataifa Jumatano, kuhusu njia ya kufikia suluhu ya mataifa hayo mawili.
Lakini serikali ya Netanyahu yenye misimamo mikali imeendelea na ujenzi wa makazi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Palestina Jambo linalochukuliwa kuwa kinyume cha sheria za kimataifa.