Benki Kuu ya Tanzania imesema Watumiaji wa Huduma za ‘Cryptocurrency’ (Sarafu Mtandao) wapo hatarini kupata hasara ikitokea kuna madhara kwenye Fedha wanazowekeza katika Mfumo huo kwa kuwa inaweza kuwa ngumu kwao kuzirejesha.
Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba ameyasema hayo akizungumza kwenye Uzinduzi wa Ripoti mpya ya FinScope Tanzania 2023, Jijini Dar es Salaam.
“Huduma za ‘cryptocurrency’ hazipo kwenye uratibu mzuri na tumekuwa tukitoa tahadhari kwa watu wanaotumia uwekezaji huo, wapo wanaopata hasara kwa kuwa kuna mifumo ya ukweli na mingine ya uwongo ndio maana tumekuwa tukitoa tahadhari kwa wanaotumia uwekezaji huo”. Amesema
“Bado mifumo yetu Nchini haijaweza kubainisha ipi ni halisi na ambayo si halisi, ndio maana hata wanaocheza wanafanya hivyo katika mazingira hayo, wajiepushe kwa kuwa hatuna mifumo ya kufuatilia, kwa maana hiyo BoT tunaendelea kufanya tafiti kwa ajili ya kupata mifumo itakayosimamia”.
Hata hivyo mpka hivi sasa takwimu zinaonesha kuna vijana 1.7% wanaona kuna fursa katika sarafu mtandao (cryptocurrency) na kushiriki kitu ambacho ni hatari.