Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuja na kampeni ya kuwatangaza kwenye vyombo vya habari wateja wake ambao wamegoma kulipa fedha wanazodaiwa.
Mpaka sasa shirika hilo linawadai wapangaji wake Sh23 bilioni fedha ambazo imeelezwa kama wangezipata zingeweza kufanyia shughuli mbalimbali za shirika ikiwemo ujenzi wa nyumba.
Akizungumza leo Jumanne Agosti 15, 2023 kuhusu kampeni hiyo iliyobeba kaulimbiu ya ‘ Lipa madeni yako kwa maendeleo ya Shirika na Taifa Letu’, Meneja Habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya amesema hatua hii ni baada ya kuelekea kuisha kwa miezi mitatu aliyoitoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha kikao cha bunge Julai 2023 ambapo aliagiza wadaiwa wote wawe wamelipa madeni yao ndani ya miezi mitatu.
“Wadaiwa sugu watakaokaidi maelekezo ya shirika watakuwa wameruhusu shirika kuwatangaza katika vyombo vya habari ili mashirika na kampuni nyingine yasiingie kwenye makubaliano ya kibiashara na mtu au kampuni inayodaiwa,” amesema.
Ameongeza kuwa ili kuweza kukusanya madeni katika kampeni hiyo shirika limemua kufanya mambo nane ikiwemo kuundwa kwa menejimenti ambayo itaanza kazi rasmi wiki hii ya kufuatilia madeni hayo.