Canada imetangaza kutoa msaada wa dola milioni 25 kwa Tanzania, zitakazotumika katika mradi wa elimu uitwao ‘Kila Binti Asome’.
Mradi huu una lengo la kuwawezesha kielimu watoto wa kike katika ngazi ya shule za msingi na sekondari za Tanzania Bara na Zanzibar.
Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dodoma katika sherehe za utiaji saini wa makubaliano hayo, kati ya Waziri wa Canada anayehusika na Maendeleo ya Kimataifa na Waziri wa Elimu wa Tanzania.
“Mradi huu utawezesha mabinti, wenye umri kati ya miaka 10 hadi 19, kujifunza na kuongeza ujuzi ili kuendana na mahitaji ya soko la sasa la ajira na baadae” amesema Waziri Harjit Sajjan.
Kwa upande wake, Profesa Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu nchini Tanzania, amesema Tanzania iko katika hatua za mwisho za kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ikiwemo kuwa na miaka 10 ya elimu ya lazima badala ya miaka 7.
“Vile vile elimu ya sekondari itajikita zaidi katika kutoa elimu ya jumla pamoja na elimu ya amali, mageuzi haya yatahitaji rasilimali nyingi,” amesema Mkenda.