Rais wa sasa wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema bila kujali matokeo ya awali ya uchaguzi yalivyokuwa lakini mshindi wa kihistoria wa uchaguzi huo ni kushinda kwa demokrasia ya Uturuki.
Erdogan alisema hayo siku ya Jana Mei 16 kupitia ukurasa wake wa twitter kuwa anaheshimu nia ya dhati ya Taifa lake ambayo iliidhinishwa kupitia sanduku la kura katika uchaguzi uliofanyika Mei 14, 2023.
Hata hivyo Raisi Endorgan amesema bado anaamini kuwa muungano wake utaibuka na ushindi katika uchaguzi wa marudio wa Mei 28 kwa kupata kura nyingi zaidi ya ilivyokuwa mwanzo.
Aidha ameshukuru na kutoa pongezi kwa watu wa Uturuki kwa kukipa chama chake cha Muungano wa Watu viti vingi katika bunge la Uturuki kwenye uchaguzi wa Jumapili, Mei 14, amesema watu wa Uturuki walithibitisha kuwa na imani na chama chake.
Hayo yote yamejiri baada ya Jana Jumatatu, Mei 15, Mkuu wa halmashauri ya kusimamia uchaguzi nchini humo kutangaza kuwa Uturuki itafanya duru ya pili ya uchaguzi Mei 28 ili kumchagua raisi baada ya kukosa mgombea aliyepata asilimia za kutosha katika uchaguzi wa jumapili.
Duru ya kwanza ya upigaji kura ilimalizika bila mgombea aliyeweza kupata kiwango cha asilimia 50 kinachohitajika, lakini Erdogan aliongoza kwa asilimia 49.51 ya kura.
Mpinzani wake wa karibu Kemal Kilicdaroglu ambae ni Mwenyekiti Mkuu wa chama cha upinzani cha Republican People’s Party (CHP) na mgombea mwenza wa Muungano wa vyama sita vya upinzani National Alliance, alipata asilimia 44.88 ya kura.