Timu ya Taifa ya Soka ya Wanawake Tanzania ‘Twiga Stars’ imepanda kwa nafasi 10 katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa mwezi Desemba.
Kwa mujibu wa viwango vilivyotangazwa juzi, timu hiyokwa sasa ipo katika nafasi ya 121 kutoka ile ya 131 ambayo ilikuwepo katika chati iliyotolewa Agosti 25, mwaka huu.
Kuwepo katika nafasi ya 121 kidunia, kunaifanya Twiga Stars kuwa kinara katika Ukanda wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ikifuatiwa na Kenya iliyo katika nafasi ya 133 na Ethiopia iliyopo katika nafasi ya 138.
Kwa Afrika, inashika nafasi ya 18 huku kinara ikiwa ni Nigeria ikifuatiwa na Afrika Kusini na Ghana ambayo inashika nafasi ya tatu.
Ushindi katika mechi mbili ilizocheza Oktoba za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON) 2026 dhidi ya Ethiopia nyumbani na ugenini unaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Twiga Stars kupata pointi 1,130 ambazo zimeipandisha zaidi.
Katika mchezo wa kwanza, uliochezwa Oktoba 22 hapa Dar es Salaam, Twiga Stars ilipata ushindi wa mabao 2-0 na Oktoba 28, ikapata ushindi wa bao 1-0 ugenini huko Addis Ababa, Ethiopia.



