Baada ya umeme kuzimika bungeni mara kadhaa wakati wa kikao cha leo Mei 15, 2023, Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limejitokeza na kufafanua kwamba kukatika huko kwa umeme hakuhusiani na laini ya Tanesco inayopeleka umeme bungeni.
Leo baada ya kipindi cha maswali na majibu kwisha, mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi alisimama kuchangia kuhusu hotuba ya Waziri wa Afya ambayo iliwasilishwa mwishoni mwa wiki.
Wakati akizungumza, umeme ukakatika na ndani ya dakika tatu umeme ulikatika kama mara mbili, wabunge wakabaki wametulia wakisubiri urudi. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson baada ya kuona hivyo akaamua kuahirisha shughuli za Bunge.
Akizungumzia kuhusu kukatika kwa umeme bungeni, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Martin Mwambene amesema laini ya umeme ya Bunge inaangaliwa kwa makini kwa kuwa hiyo ni taasisi nyeti na inapewa kipaumbele kama vile hospitali.
Amesema watu wamekuwa wakihusisha kila kukatika kwa umeme na Tanesco, jambo ambalo amesema siyo kweli kwa sababu wajibu wa Tanesco unaishia kwenye mita, lakini ukiingia ndani, ni eneo linalomhusu mteja.