Kiongozi wa upinzani wa Senegal, Ousmane Sonko, hana mpango wa kutafuta maridhiano na Rais Macky Sall, na ameshiria kuwa anaweza kuvuruga uchaguzi wa mwaka ujao, ikiwa hataruhusiwa kugombea.
“Hakutakuwa na uchaguzi katika nchi hii, iwapo Rais Macky Sall atapinga kugombea kwangu,” Sonko alisema hayo akiwa nyumbani kwake katika mji mkuu wa Dakar ambako amekuwa chini ya kizuizi cha nyumbani tangu alipohukumiwa kifungo cha miaka miwili mwezi Juni, kwa mashtaka yaliyotokana na madai ya ubakaji.
Sonko alikanusha mashtaka hayo na kusema kuwa yanalenga kumzuia kushiriki katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwezi Februari mwakani.