Maelfu ya watu nchini Niger, wameandamana kwa siku tatu mfululizo katika mji mkuu wa Niamey, wakiitaka Ufaransa kuondoa wanajeshi wake, kama inavyotaka serikali ya kijeshi, iliyochukua mamlaka mwezi Julai.
“Ufaransa ishindwe! Ufaransa, iondoke,” ni maneno ambayo waandamanaji hao waliimba, wakirudia kauli mbiu zilizosikika katika mikutano mbalimbali, tangu mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 26 mwezi Julai.
Utawala wa kijeshi wa Niger, uliishutumu Ufaransa kwa kile ulichokiita uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa kumuunga mkono Rais aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum.
Tangu wakati huo, maelfu ya watu wameshiriki maandamano kwenye mzunguko wa barabara, karibu na kambi ya kijeshi ya Niger, ambapo wanajeshi wa Ufaransa wameweka kambi.
Uhusiano na Ufaransa, mshirika wake Niger katika mapambano dhidi ya ugaidi, ulizorota haraka baada ya Ufaransa kusimama na Rais aliyeondolewa madarakani.