Serikali imeanza mchakato wa ujenzi wa barabara ya kuunganisha Kibaha na Chalinze katika Mkoa wa Pwani kwa kujenga barabara ya kasi baina ya maeneo hayo mawili.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu kiasi cha dola za marekani milioni 340 (Shilingi za Tanzania bilioni 833).
Muwekezaji wa mradi huo anatarajiwa kujulikana mwezi Machi mwaka 2024, kwani sasa hivi kuna mchakato wa kuchagua kutoka kampuni 5 zilizoomba zabuni hiyo.
Serikali imepanga kutekeleza mradi wa barabara ya kasi ya kilomita 205 Kutoka Kibaha hadi Morogoro, kwa sehemu mbili kwa mfumo wa ushirikiano wa umma na binafsi (PPP).
Sehemu hizo ni kilomita 78.9 kati ya Kibaha na Chalinze na kilomita 126 kati ya Chalinze na Morogoro.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa njia nne za barabara kutoka Kibaha hadi Morogoro.
Pamoja na mradi huo, pia serikali imeweka mpango wa kujenga barabara ya njia mbili, kutoka Morogoro hadi Dodoma.
Wakati akisoma bajeti ya mwaka 2023/24 ya wizara ya Uchukuzi, Waziri Makame Mbarawa alisema wizara yake inafanya tathmini ya wakandarasi walioomba zabuni kwa kutoa maoni ya mradi.
Waziri wa Uchukuzi alisema katika Mkutano wa 15 Mapitio ya Sekta ya Usafiri mwezi Novemba 2022, kuwa “muwekezaji binafsi atachangia fedha za kukamilisha mradi na pia kusimamia uendeshaji wake yaani “Build Operate” na kuongeza kuwa ujenzi wa mradi huo utakwenda sambamba na unejzi wa barabara kuu ya sasa.
“Muwekezaji atatoza ada ya kupita kwa wale wanaotaka kutumia barabara hiyo ya kasi kwa hiari, kwani barabara kuu ya sasa bado itaendelea itatumika,” alisema.
Kamishna wa PPP katika Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. David Kafulila, alitaja kampuni tano zilizochaguliwa kushiriki katika zabuni hiyo.
Kampuni hizo ni muunganiko wa makampuni ya M/s CRCC-CCECC-CRCCIG na M/s Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation Ltd.
Na kuongeza nyingine ambazo znajitegemea ni M/s Yunnan Construction and Investment Holding Group Co. Ltd; M/s Yapi Merkezi Insaat ve Sanayi A.S na M/s Egis Projects SAS JV na M/s China Communications Construction Co. Ltd (CCCC).
“Kampuni tano zilichaguliwa kati ya tisa ambazo ziliwasilisha Maombi ya Kustahiki (RFQs). Kulingana na matokeo ya tathmini, makampuni haya tano yaliyoteuliwa yatapewa Maombi ya Pendekezo (RFP) na wanatakiwa kuyawasilisha serikalini kabla ya mwisho wa Novemba mwaka huu,” Bw. Kafulila alisema.
“Kufikia Machi 2024, kampuni itakayotekeleza mradi wa Kibaha-Chalinze itajulikana baada ya kampuni hizo kushindana,” aliongeza.
Katika kikao na wawekezahi kilichofanyika tarehe 16 Agosti 2023, Bw. Kafulila aliwaambia wawekezaji 40 kwamba M/s Cheil Engineering Co Ltd kwa kushirikiana na Korea Expressway Corporation, Hana E&C Co Ltd, Afrisa Consulting na ENGTEC Tanzania Ltd walikuwa washauri wa mchakato wa mradi.
Bw. Kafulila alisema kazi ya washauri hao ni kuisaidia serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) katika maandalizi ya mradi huo.
“Hii ni kuhakikisha kuwa miradi yote ya PPP inaandaliwa na kampuni zenye uwezo na sifa za kimataifa ili kupata nyaraka za mradi zenye ubora,” alisema.
Hivyo, aliwataka wawekezaji kuwasilisha mapendekezo ya miradi isiyoombwa kwa sehemu za Chalinze-Morogoro na Morogoro-Dodoma, akibainisha kuwa hii iliruhusiwa kisheria.
Akaongeza kwa kusema kuwa hakuna haja ya kusubiri mapendekezo yaliyoombwa yanayotayarishwa na mamlaka ya serikali.
Hadi sasa haijafahamka mradi wote utatumia muda gani kukamilika, ila kipande cha Kibaha chalinze kinatazamiwa kujengwa kwa miaka mitatu.
Wawekezaji hao wanatarajiwa kupewa msamaha wa kodi kutokana kadiri sheria za uwekezaji zitakavyoruhusu kulingana na miongozo ya Kituo cha Uwekezaji (TIC)
hatua hii ya serikali kuhusisha sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya kimkakati kama barabara, reli, viwanja vya ndege na bandari utaharakisha ujenzi nchini, na kutoa fursa ya ajira kwa wananchi.