Mtoto wa miaka miwili ametolewa sarafu iliyokwama kooni kwake kwa muda wa siku sita katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) jijini Dodoma.
Akizungumza hapo Jana Aprili 3, 2024 Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo (ENT) wa BMH, Emmerenceana Mahulu, amesema walimpokea mtoto huyo Machi 26, 2024
“Tumefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto kwa siku sita kwa kutumia kifaa tiba kinachoitwa ‘esophagoscopy’,” amesema Mahulu
Amesema, sehemu ya koo ilipokuwa imekwama sarafu ilisababisha uvimbe na kuacha uwazi kidogo ambao uliruhusu vimiminika kama uji, maji juisi kupita.
“Mtoto anaendelea vizuri baada ya matibabu na anaweza kula vizuri kwa sasa. Tumeshamruhusu na tutamuona tena baada ya wiki moja ili kuona maendeleo yake,” amesema.
Mama wa mtoto Bi. Juliana Yuda, mkazi wa Kijiji cha Mkoka, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, amesema mtoto wake ambaye alitoka kucheza na wenzake siku ya Jumamosi ya Machi 20, alirudi nyumbani muda wa mchana akiwa analia.
“Mtoto alikuwa hawezi kula kwa muda wa siku sita, alikuwa anashindia uji, juisi na maji tu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya siku ya Alhamisi,” amesema.
Amesema awali alimpeleka mtoto huyo katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa ambapo alipewa rufaa kuja BMH baada ya kupigwa picha ya x-ray na kubaini sarafu imekwama kwenye koo.