Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ameandika barua kwa viongozi wa nchi wanachama wa G20 akitoa pendekezo la Umoja wa Afrika kupewa uanachama kamili na wa kudumu katika kundi hilo la kidiplomasia katika mkutano unaotarajiwa kufanyika nchini India mwaka huu.
Pendekezo la Modi la kuupa Umoja wa Afrika uanachama kamili wa G20 linaonyesha azma ya India ya kuimarisha uwakilishi na ushirikiano wa Afrika katika masuala ya kimataifa.
Chanzo cha taarifa hizi kimesema kuwa kiongozi huyo wa India ni hupendelea nchi zinazoendelea kuwa na sauti ya kusema katika majukwaa ya kidunia na kuongezea kuwa “Hii itakuwa hatua sahihi kuelekea muundo na utawala wa kimataifa wenye haki, usawa, wenye kujumuisha zaidi na uwakilishi”.
G20 ni jukwaa la kiserikali la mataifa yaliyoendelea na mataifa yanayoendelea. Nchi wanachama wanakusanya takriban 85% ya pato la dunia, zaidi ya 75% ya biashara ya kimataifa, na karibu theluthi mbili ya idadi ya watu duniani.
Kundi hili lina mataifa wanachama 19 na Umoja wa Ulaya. Miongoni mwa mataifa yaliyoalikwa katika mkutano wa mwaka huu nchini India ni Bangladesh, Singapore, Uhispania, na Nigeria, pia yamealikwa mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya Duniani, Benki ya Dunia, na IMF.