Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa asasi ya TAHIA kutafakari juu ya kuwa na mfumo mmoja wa taarifa katika vituo vyote kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa mpaka kwenye zahanati ili kusaidia kuokoa gharama za matibabu kwa mwananchi anayehitaji huduma hasa katika kipindi cha Rufaa.
Dkt. Mollel amesema hayo Jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa Asasi ya Tanzania Health Information Agency (TAHIA) inayoundwa na wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano yenye lengo la kuweka rasilimali watu pamoja, rasilimali fedha ili kwa pamoja kuondoa changamoto iliyopo ya mifumo mingi inayoshindwa kubadilishana taarifa kutoka kituo kimoja kwenda kingine.
Amesema, mfumo huo wa taarifa za mgonjwa utaokuwa unasomana, utahusisha mpaka taarifa za fedha katika vituo, lakini pia huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wanaotumia bima ya afya ni jambo litalosaidia kuboresha huduma kwa wananchi na kupunguza upotevu wa mapato katika vituo vinavyohudumiwa na watumishi wasio waadilifu.
Aidha, Dkt. Mollel amesema kuwepo kwa mfumo mmoja unaosomana katika sekta ya Afya kutasaidia kuboresha matumizi ya taarifa (data) katika ngazi ya vituo na katika ngazi ya viongozi wa juu wa sera ili kusaidia kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kwenye eneo la kutenga fedha.