ZINAZOVUMA:

Uchambuzi uzinduzi wa ikulu chamwino

Uzinduzi wa Ikulu ya Chamwino Dodoma, umeleta mengi ikiwemo tafsiri...

Share na:

Anaandika Dkt Ahmad Sovu.

HATIMAYE HISTORIA IMEANDIKWA! DKT. SAMIA AZINDUA IKULU YA CHAMWINO-DKT. MPANGO ASEMA HII NI LULU, DKT. JK SI YA MWAYANGU MWAYANGU IMEKAMILIKA HASWA

Uchambuzi wa Tukio hilo adhimu na miradi 10 kama ilivyodadavuliwa na Katibu mkuu Kiongozi, Dkt. Mozes Kusiluka.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania- Kazi Iendelee

Ni historia ya pekee imeandikwa, ambapo ndoto ya muasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kutaka Makao makuu ya chama na serikali yawe Dodoma imetimia, ambapo hivi leo Mei 20, 2023 Mheshimiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan ameizindua rasmi ikulu hiyo.👏👏

Kama alivyosema mwenyewe Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa;

Napenda Kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kutufikisha siku ya leo na kushuhudia tukio hili kubwa la kihistoria katika Taifa letu, ni tukio adimu na adhimu na lenye kuleta faraja kwa kuwa kwa mara ya kwanza, Watanzania tumeweza kujenga ikulu yetu, kwa kutumia rasilimali zetu na kutumia wataalamu wetu wa Kitanzania

Kwa hakika ni jambo la faraja sana kushuhudia uzinduzi wa ikulu yetu wenyewe.

Pamoja na kuelezea historia ya mchakato wa ujenzi huo hadi ukamilifu wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefafanua kuwa kila awamu ya uongozi imekuwa na mchango wake katika kukamilisha ujenzi wa ikulu hiyo.

Mathalan, baadhi ya hatua zilichukuliwa na awamu za nyuma ni pamoja na

  • Ujenzi wa nyumba za muda za serikali,
  • Ujenzi wa makao makuu ya CCM,
  • Bunge la JMT,
  • Ofisi za TAMISEMI,
  • Chuo Kikuu cha Dodoma
  • Hospitali ya Benjamin Mkapa,
  • Ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete n.k

Na hadi ilipofikia tarehe 23/7/2016 Rais Magufuli alikumbusha katika mkutano mkuu CCM Taifa ambapo upanuzi na uendelezaji wa ikulu ya CHAMWINO ulianza.

Kukamilika kwa ujenzi huu umeambatana na kukamilika miradi mbalimbali iliyopo ndani ya Dodoma na nje ya Dodoma kwa shabaha ya kuhakikisha lengo la kuhamia Dodoma linafikiwa bila ya changamoto nyingi.

Kama alivyofafanua katibu mkuu kiongozi Ndugu Dkt. Kusiluka.

Dkt. Kusiluka aichambua Falsafa ya kazi iendelee kwa kudhihirisha miradi 10 iliyotekelezwa

Awali alipokuwa akitoa taarifa ya mradi huu, katibu mkuu kiongozi Mheshimiwa Dkt. Mozes Kusiluka amebainisha kuwa Rais Dkt. Samia amekuwa akitekeleza salamu yake ya Kazi iendelee kwa vitendo,
ambapo ameendelea kusimamia kukamilisha miradi hiyo.

Baadhi ya miradi hiyo aliyoiendeleza ni pamoja na hii ifuatayo;

1. Ujenzi wa Ikulu ya Chamwino Dodoma

2. Ujenzi wa majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za serikali pamoja na miundombinu mingine kwenye mji wa serikali wa Mtumba. Ambapo amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia 70 na utekelezaji wake unatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 700

3. Ujenzi wa makao makuu ya mahakama ya Tanzania ambao umekamilika kwa asilimia 91 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 129.7

4. Kukamilika kwa ujenzi wa reli ya kisasa, yaani SGR kuanzia kukamilika kwa vipande viwili kile cha DAR Morogoro na Morogoro Makutupora ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90 kwa vipande vyote

5. Mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere ambapo wakati Dkt.Samia Suluhu Hassan anashika hatamu ulikuwa umekamilika kwa asilimia 31.6 na sasa umefikia asilimia 86.8. Mradi huu umetuma Trilioni 6.5 na hadi mwezi Aprili mwaka huu wakandarasi wamelipwa Trilioni 5.3 na hadi sasa serikali haidaiwi

Miradi Mipya
Kwa upande wa miradi mipya, Mheshimiwa Dkt. Kusiluka alisema Dkt. Samia ameanzisha miradi mipya ndani ya miaka 2 ya uongozi ambayo ni;

1. Mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato Dodoma ambao utatumia gharama zaidi ya Bilioni 360.

2. Mradi wa ujenzi wa Barabara ya mzunguko (Ring Road) yenye urefu wa Kilomita 112.3 jijini Dodoma ambao utagharimu Shilingi Bilioni 221.7

3. Ujenzi wa Barabara kuu zenye urefu wa Kilomita 471.5 kazi inandelea

4. Bajeti ya ujenzi imeongezeka na matengenezo ya barabara za vijijini na mijini kutoka Bilioni 275 hadi Bilioni 900 za barabara ya lami jumla ya Kilomita 765

5. Kuongeza vipande vya SGR kutoka Makutupora mpaka Tabora Issaka na Mwanza, pia ujenzi wa SGR kutoka Tabora hadi Kigoma. Jumla ya vipande vyenye urefu wa Kilomita 1380 tayari ujenzi umeanza. Jumla ya Trilioni 23.3 hadi sasa zimetumika.

Hivi ndivyo alivyotafsiri kwa vitendo falsafa ya kazi Iendelee Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo Mheshimiwa Katibu mkuu amesema hii ni miongoni tu mwa miradi ambayo ameianzisha na kuendeleza.

Dkt. JK amsifu Dkt. Samia amefanya makubwa

Kwa niaba ya viongozi wastaafu Mheshimiwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho alielezea kwa muhtasari historia ya ujenzi wa ikulu hiyo, Mheshimiwa JK pia alimpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilishwa ujenzi huo ambao leo umezinduliwa.

Aidha, amempongeza kwa kazi kubwa anayofanya ya kutekeleza miradi mikubwa iliyoanzishwa na mtangulizi wake na ambayo ameianzisha yeye mwenyewe. Alisema;

Mwenye macho haambiwi tazama, miradi mikubwa umeitekeleza

Mheshimiwa JK alisisitiza kuwa ujenzi huu umekalika vizuri na sio wa kimwayangu mwayangu🤣🤣 yaani, haujakaa sawa ila huu umekamilika na umemjengea heshima Mheshimiwa Rais mama yetu Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Katika hatua nyingine Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, pamoja na pongezi alimshukuru sana Dkt.Samia kwa Zanzibar kupata eneo la kujenga ofisi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jijini Dodoma ikiwa ni pamoja na kutengewa ofisi katika ikulu hiyo.

Kwa upande wake, Mwanamazingira ambaye pia ni makamu wa Rais Dkt.Philip Isdory Mpango aliwataka watendaji wa ikulu kutunza vema mazingira mazuri ya ikulu hiyo.

Yajayo yanafurahisha

Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ataendeleza yote ya mtangulizi wake na kuleta mengine mapya. Alisema;

Nitaendeleza, Nitaboresha na kuleta mengine

Alisema mradi wa kwanza kuukamilisha ni ule wa Daraja la Tanzanite jijini Dar es Salaam na huu wa ikulu Chamwino.

Aidha, amesema katika eneo hilo la Ikulu pia bado kuna kazi ya kufanya ambapo itajengwa SAMIA COMPLEX itakayokuwa na;

  • Ukumbi wa mikutano unaoweza kuchukua watu 2000 hadi 3000.
  • Nyumba za viongozi majirani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC
  • Zanzibar Lounge
  • East African Lounge
  • Uwanja wa Golf
  • Njia ya ndege
  • Viwanja Mbalimbali vya michezo
  • Sehemu za Historia za viongozi wetu na nchi yetu na kadhalika.

Mheshimiwa Rais Samia amesema michoro ipo tayari ilobaki ni kutafuta fedha tu.

Kwa hakika leo historia imeandikwa kama ilivyosema Mheshimiwa JK imeandikwa tena kwa wino wa dhahabu

Kukamilika kwa ujenzi wa ikulu hii, kama alivyosema Mheshimiwa Rais Dkt.Samia sasa ile ndoto ya baba wa Taifa imetimia na Dar itabaki kwa ajili ya shughuli za kibiashara na mambo mengine machache ya Kiserikali yanatakiwa kufanyika huko.

Hakika jambo hili ni jema sana na labda ninukuu kwa uchache beti kutoka katika wimbo ulioimbwa na Msanii Mrisho Mpoto maarufu kama mjomba katika uzinduzi huo pale alipoimba;

Nataka mjue Historia
Hii sio ya Kurithi
Hii ni ya kwetu
Tumejenga wenyewe
Oohh My God

Nakshi, sura, ukamilifu
Tumpe nani Kongole?
Yule pale, yule pale
Yule pale mwenye sauti ya umoja, uadilifu na upambanaji
Daktari Samia Suluhu Hassan
Mbeba maono na mkamilishaji wa ndoto…

Kwa hakika Mheshimiwa Dkt.Samia anastahili kongole sana kwa kuchaguliwa na mola kuwa mkamilishaji wa ujenzi huu na kuwa Rais wa kwanza kutumia ikulu hii.

Kongole pia kwa JKT, TBA na wazalendo wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine ukamilishaji wa ikulu hii.

Kwa hakika mmemuheshimisha Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kumvika koja lenye lulu na kila nuru ya kuvutia. Kongoleni sana 👏👏👏

Sasa Dodoma kweli ya Watanzania chambilecho mzee Chidumule. Ndoto imetimia kazi IENDELEEE.

Nimalizie kwa dua kwa Dkt.Samia kama ilivyosomwa na waghani wa utenzi mabanati kutoka Zanzibar pale waliponena;

Mungu akupe wepesi
Kipenzi chetu Rais
Akulinde na Nuhusi
Hasadi na Mabalaa…. Amina.

Mwandishi ni Mhadhiri na Mshititi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya Kivukoni DSM.

sovu82@gmail.com
0713400079

Endelea Kusoma

Uchambuzi wa Maeneo ma 3 muhimu ya Kitajriba katika uteuzi huu wa

Chaguo la Mhariri

Habari Mpya