Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Kenya, ametoa amri ya kukamatwa kwa waziri wa Kilimo wa Mithika Linturi na Katibu Mkuu wa wizara ya Kilimo Paul Ronoh.
Sababu ya kukamatwa kwa vigogo hao wa Kenya, ni sakata la mbolea feki linaloendelea nchini humo.
Ofisi ya DPP siku ya Alhamisi iliidhinisha mashtaka dhidi ya wawili hao, baada ya uchunguzi uliofanywa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).
Hii pia inafuatia kukamatwa wakurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), na kupandishwa kizimbani ambapo walikiri mashtaka siku ya Alhamisi na kuachiwa kwa dhamana.
Linturi alihojiwa na makachero siku ya Ijumaa iliyopita, Makao Makuu ya DCI huko Kiambu ambapo alikanusha kuhusika na sakata hilo.
Wabunge siku ya Alhamisi walipiga kura kuunga mkono kung’olewa kwake madarakani, hadi sasa hatma yake ipo mikononi mwa kamati teule itakayochunguza tuhuma dhidi yake.