Hospitali ya Benjamin Mkapa imeanza kufanya upandikizaji uume na imetaja gharama za kupandikiza kuwa ni kati ya Sh6 milioni hadi Sh10 milioni.
Hayo yamesema leo Jumanne Agosti Mosi mwaka 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt Alphonce Chandika wakati akielezea vipaumbele vya bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Dkt Chandika amesema huduma hiyo imeanzishwa baada ya kubaini kuwa kuna changamoto kubwa ambayo imewafanya wanaume wengi kuhangaika wengine hata kutapeliwa na waganga wa kienyeji kwa dawa za uongo.
“Sisi kama taasisi ya umma tukaona kwanini tusije na mkakati wa kuwasaidia hawa watu wenye changamoto kwenye nguvu za kiume. Kwa maana hiyo tulianza kutoa hii huduma kwa kutoa huduma kwa wanaume wawili,” amesema.
Amesema habari njema kutoka kwa wanaume hao, mambo yamekuwa mazuri na kwamba waliwapa masharti kuwa waanze kufanya tendo la ndoa wiki sita baada ya kufanyiwa upasuaji.