Serikali ya Kenya ipo kwenye mpango wa kuuza sehemu ya hisa zake katika kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, huku ikisukuma pia mpango wa kuigawa kampuni hiyo na kuwa kampuni tatu tofauti.
Kupitia mpango huo, Safaricom inatarajiwa kugawanyika na kuunda kampuni ya minara ya simu, kampuni ya mawasiliano, pamoja na kampuni ya teknolojia ya fedha (Fintech). Serikali inaamini kuwa mgawanyiko huo unaweza kuongeza thamani ya kampuni zaidi ya ilivyo sasa.
Mpango wa kuuza hisa bado unaendelea kujadiliwa, ambapo serikali inalenga kuuza asilimia 15 ya umiliki wake. Waziri wa Fedha wa Kenya, John Mbadi, amesema kuwa endapo mauzo hayo yatatekelezwa, kampuni ya Vodacom Afrika Kusini itabaki na umiliki wa asilimia 55 ya Safaricom.
Kwa mujibu wa Mbadi, mauzo ya hisa hayo yanatarajiwa kuiingizia serikali ya Kenya mapato yanayokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 2.4.
Ameongeza kuwa mpango wa kuigawa Safaricom utawezesha kampuni hiyo kuimarisha shughuli zake za teknolojia ya fedha, pamoja na kupanua wigo wa biashara katika nchi nyingine barani Afrika, kufuatia hatua za awali zilizochukuliwa nchini Ethiopia.



