Tume ya Ushindani (FCC)
imewataka wafanyabiashara wa Kariakoo mkoani Dar es Salaam, kujiridhisha katika vyanzo vya kuaminika kuhusu ubora wa bidhaa wanazoagiza kabla ya kuanza kuziuza nchini ili kuondoa wimbi la bidhaa bandia.
Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio alisema hayo mkoani Dar es Salaam jana baada ya kumaliza kikao na uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo kilichofanyika kwenye ofisi ya tume hiyo.
“Ili kujua kuwa bidhaa ni bandia au la mfanyabiashara anapaswa kujua chanzo halali kinachozalisha bidhaa na bei halali,” alisema.
Erio alisema wafanyabiashara wanapokwenda kununua bidhaa nje ya nchi ili kujiridhisha ni vyema wakafika kwenye balozi za Tanzania ili kujiridhisha uhalali wa wazalishaji na ubora wa bidhaa husika.
“Si kwamba wafanyabiashara hawajui kuwa bidhaa wanazotumia ni bandia, ila wanavutiwa na bei ndogo ndio maana wananunua bidhaa bandia au zilizoghushiwa,” alisema.
Erio alitolea mfano wa udhibiti wa bidhaa bandia waliofanya katika bandari mwaka wa fedha 2022/23, wamefanikiwa kudhibiti bidhaa bandia kwa asilimia 97 na wanaendelea kudhibiti kwa kuwachukulia hatua za kisheria waliokutwa na bidhaa bandia ili kuhakikisha hakuna bidhaa bandia inayoingia nchini.