Israeli yashambulia Iran kwa makombora alfajiri ya Ijumaa, vimeripoti vyombo vya habari vya Marekani, vikiwanukuu maafisa wa juu katika utawala wa Biden ambao hawakutajwa majina.
Ripoti za mashirika ya habari ya ABC, CBS na NPR hazikutoa maelezo zaidi kuhusu eneo au lengo la shambulio hilo la kombora.
Msemaji wa jeshi la Israel aliiambia VOA kuwa hana maoni yoyote “kwa sasa” kuhusu ripoti za vyombo vya habari vya Marekani, takriban saa moja baada ya ripoti hizo kutokea.
Shirika la habari la serikali ya Iran IRNA limesema ulinzi wa anga wa jamhuri ya Kiislamu umeanzishwa angani katika majimbo kadhaa.
Shirika la IRNA na shirika jingine la serikali la Fars, lenye mafungamano na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, yamenukuu vyanzo vya habari ambavyo havikutajwa vikisema kuwa “kumetokea mlipuko katika mkoa wa kati wa Iran wa Isfahan.”
Fars walipata mlipuko huo katika mji wa Qahjaverestan, viunga vya mashariki mwa mji wa Isfahan.
Israel ilikuwa imeionya Iran kwamba italipiza kisasi kwa shambulio la anga la Iran dhidi yao, ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel Jumapili iliyopita.
Iran ilikuwa imeonya, kwa upande wake, kwamba hatua yoyote ya kulipiza kisasi ya Israel ingekabiliwa na jibu la haraka na kali zaidi.
Vyombo vyote vya habari duniani vimeelekeza macho na masikio katika Mzozo huu mpya baina ya Iran na Israel.