Waziri wa Ulinzi wa Iran amethibitisha kuwa jitihada za kununua ndege za kivita kutoka Urusi zimegonga mwamba.
Waziri huyo ambaye pia ni Brigedia Jenerali wa jeshi la ardhini la Iran, amesema hayo na kusisitiza kuwa zinaweza kuzalishwa ndani kwa kuwa wana uwezo huo.
Waziri huyo hakutaka kutoa taarifa Zaidi ila alisema kuwa, “hapo mwanzo walikuwa na mpango huo, ila tumeamua kuzalisha ndege hizo nchini kwetu” na kuongeza kuwa mbali na nia ya kuzalisha pia wanaendelea na uchunguzi ili kuona kama kuna haja ya kuendelea na mpango wa kununua.
Tayari kuna taarifa kuwa Iran imeanza kuzalisha ndege hizo mwaka 2018, huku baadhi ya wachambuzi wa kijeshi wakisema wanazalisha ndege mithili ya ndege za miaka ya 1960 za Marekani, modeli ya F5.
Muandishi wa masuala ya anga, Babak Taghvaee amesema, sababu kuu ya kushindikana kwa mauziano hayo ni msimamo wa Urusi wa kutokutoa teknolojia muhimu za ualishaji wa ndege hizo.
Babak pia anasema “Uongozi wa jeshi la Iran umegoma kununua ndege hizo, sababu Urusi iligoma kutoa teknolojia ya kutengeneza vipuri muhimu vya ndege hiyo kwa Iran, kwa muda wa miaka 30 ijayo”.
Mbali na msimamo huo wa jeshi la Iran, baadhi ya watu wanaamini kuwa Israel ina mkono wake katika kushawishi kuzuia Urusi isitoe teknolojia hiyo kwa Iran, wakiamini kuwa ushirikiano huo wa kijeshi unaweza kuwa na hatari kwa Israel.