Afisa nchini Libya amesema inaaminika kuwa mpaka hivi sasa zaidi ya watu 5,300 wamepoteza maisha baada ya mafuriko katika mji wa Derna nchini humo.
Ingawa bado idadi haijawa rasmi lakini kila baada ya muda miili imekua ikiokotwa kutoka baharini hivyo kuongeza idadi ya waliopoteza maisha mashariki mwa Libya.
Kumekuwa na wito wa kuhitaji msaada zaidi wa kibinadamu ili kuwaokoa waathiriwa ambao bado wapo hai na kufanikisha kuwazika waliopoteza maisha ambao wanazikwa kwenye makaburi ya pamoja.
Vikosi vya uokoaji vinachimba vifusi vya majengo yaliyoporomoka kwa matumaini ya kupata walionusurika lakini matumaini yanafifia na idadi ya waliofariki bado inatarajiwa kuongezeka zaidi.
Maafisa wanasema takribani watu 10,000 hawajulikani walipo, huku watu 30,000 wakikadiriwa kuwa wameyahama makazi yao.