Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameondoa pingamizi kwa Sweden kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (Nato) na kuahidi kuwa atawasilisha uamuzi huo haraka iwezekanavyo ili upitishwe na Bunge la Ankara.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Nato, Jens Stoltenberg aliyefanya mazungumzo na Erdogan pamoja na Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson, japokuwa taarifa ya pamoja iliyotolewa na viongozi hao watatu haijabaini ni kwa muda gani Bunge la Uturuki linalazimika kuidhinisha ombi hilo la Sweden.
Stoltenberg amesema kukamilika kwa ombi la Sweden ni hatua ya kihistoria inayonufaisha usalama wa washirika wote wa Nato.