Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar itaendelea kuwa muumini wa dhati wa Muungano, kwa kudumisha na kuimarisha kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yaliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mwinyi amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kupata sifa na heshima kubwa kimataifa kwa kuwa nchi ya mfano kwa kudumisha Muungano.
Pia Dkt. Mwinyi amesema Tanzania imepata mafanikio makubwa yaliyotokana na Muungano katika sekta mbalimbali za Kiuchumi pamoja na huduma za kijamii.
Aidha amewashukuru viongozi wa awamu zilizopita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada za kudumisha Muungano pamoja kutatua changamoto zinazojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi.