Nchi ya China imetoa tangazo la kupiga marufuku bidhaa zinazotengenezwa na kampuni ya teknolojia ya Marekani, Micron Technology na kusema kuwa ni hatari kwa usalama wa taifa.
Mamlaka ya udhibiti wa anga ya mtandao nchini humo ilitoa tamko hilo siku ya Jumapili kwamba kampuni hiyo ambayo ni mtengenezaji mkuu wa chipu nchini Marekani ni hatari kubwa kwa usalama wa mtandao wa China.
Hatua hii inamaanisha kuwa chipu za kampuni hiyo zitapigwa marufuku kushiriki katika miradi muhimu ya miundombinu katika nchi ya China ambayo uchumi wake ni wa pili kwa ukubwa duniani.
Hii ni hatua ya kwanza kubwa ya China dhidi ya kampuni hiyo kubwa ya teknolojia ya Marekani, huku mvutano ukiongezeka kati ya Beijing na Washington, Marekani.