ZINAZOVUMA:

BASUTA yatoa tamko kuhusu mkataba wa bandari

Baraza kuu la Jumuiya ya Ansaar sunnah Tanzania BASUTA imetoa...

Share na:

Baraza kuu la Jumuiya za Ansaar Sunnah Tanzania (BASUTA) limetoa tamko kuhusu mkataba baina ya serikali ya Jamuhuri Muungano wa Tanzania na serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji wa bandari ya Tanzania.

BASUTA imesema Kwa kuwa katiba ya nchi yetu ya mwaka inatoa haki ya kila mtu kuwa na uhuru wa kuwa na maoni yake na kutoa nje mawazo yake na kama ambavyo kuwa watu wengine wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wanataaluma, wanahabari na wadau wengine wamekuwa wanatoa maoni yao kuhusu suala la Mkataba baina ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari Tanzania kupitia kampuni ya DP World inayomilikiwa na serikali ya nchi hiyo.

Hivyo BASUTA kwa kujali maslahi mapana ya taifa imeamua kutoa tamko kuhusu mwenendo wa mjadala wa Mkataba huo wa bandari, kama ifuatavyo;

“Kwa kuwa, tunaamini Serikali kupitia wataalamu wake imetoa ufafanuzi wa kutosha kwa wadau wanaokosoa baadhi ya vifungu vya Mkataba huo na hivyo kutaka yafanyike maboresho na kundi jingine (ambalo hatukubaliani nalo) linalopinga Mkataba wote”

“Na kwa kuwa wanaopinga Mkataba wote na kutaka ufutwe, walifungua kesi Mahakama Kuu ya kuomba tafsiri ya kisheria ambayo, kama utawala sheria unavyotaka, ilisikilizwa kwa haki na uwazi, kisha hukumu kutolewa kwamba, licha ya kasoro ndogo ndogo Mkataba huu ni halali kwa mujibu wa sheria za nchi na unaweza ukaendelea.

“Na kwa kuwa serikali sikivu ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Dr Samia Suluhu Hassan imeahidi kusikiliza na kurekebisha kasoro zote zilizoainishwa kwa maslahi ya taifa.

“Hivyo basi, sisi BASUTA tusingependa kujikita kwenye mjadala wa vipengele mahususi wa Mkataba wenyewe wa bandari tukiamini mchakato unaenda vizuri na maslahi mapana ya taifa yatafikiwa”.

BASUTA imesema haitaki kugusa vipengele vya mkataba kwa kuwa inaamini kuwa mkataba upo sawa na ina imani na serikali inayoongozwa na Rais Samia.

Lakini BASUTA imesema hairidhishwi na undumilakuwili na ukosefu wa uadilifu wa wapingaji wa Mkataba ambao walifumbia macho mikataba mingi na ya hovyo zaidi huko nyuma katika sekta mbalimbali, ikiwemo madini, na hawakutaka ifutwe; lakini wako tayari kwa gharama yoyote kuhakikisha Mkataba huu unafutwa na unakufa.

“Wanasahau kuwa huu si Mkataba wa kwanza wa ukodishaji wa uendeshaji bandarini, bali awali ilipewa jukumu hilo kampuni ya TICS na kufanya kazi hiyo kwa miaka takriban 22. Hadi TICS inaondoshwa, hakujawahi kuwa na mijadala ya hisia kama hii kupinga sera za uwekezaji na eti kutaka Watanzania wenyewe ndio waendeshe rasilimali zao, kama lilivyodai kanisa Katoliki na wadau wengine”.

“BASUTA tunatambua na kuheshimu haki ya makundi ya watu wakiwemo wanasiasa, madhehebu ya dini, wasomi na wanahabari, kuwa na maoni, lakini haturidhishwi na baadhi ya hoja za kibaguzi dhidi ya Uarabu, na hata Uislamu zinazotolewa na makundi yanayotaka Mkataba huu wa bandari ufutwe”.

Aidha BASUTA pia imesikitishwa na kitendo cha watu kutaka kutishia kuipindua serikali ya Tanzania.

Pia BASUTA imeiomba serikali kufanya mapitio ya mikataba mingine isiyo na ukomo, ikiwemo ule ulioingiwa mwaka 1992 kati ya Serikali na makanisa (Memorandum of Understanding) ambapo sehemu ya mabilioni ya walipakodi, hata wasio Wakristo, hutolewa na serikali kwa ajili ya hospitali na vyuo vikuu vya makanisa hayo.

” Pia, tunataka makubaliano yanayozungumzwa mara kwa mara kati ya serikali na kanisa ya kutojengwa hospitaliza umma mahali zilipo hospitali za makanisa yafutwe kwa sababu wananchi wana Mkataba na Serikali kuwafikishia huduma za jamii kwa gharama wanayoweza kuzimudu na sio kanisa”.

Mwisho kabisa BASUTA wamemaliza kwa kusema;

“Kwa maslahi ya umoja, mshikamano, utulivu na ustawi wa nchi yetu, tumetoa tamko letu hili kwa nia njema kabisa kwa maslahi ya nchi yetu na Watanzania wote pasina kujali dini, rangi, kabila, jinsia wala tofauti zao za kisiasa. Tanzania ni kubwa kuliko sisi sote na wala baadhi yetu wasijitwishe ukiranja wa kuwasemea wengine ilhali wako hai na wanazo haki za kiraia kama walizo nazo wao”.

Endelea Kusoma

Mwanzilishi wa Telegram mwenye asili ya kirusi amekamatwa nchini Ufaransa siku ya

Chaguo la Mhariri

Habari Mpya